Saturday, July 9, 2011

Sudan Kusini

Sudan Kusini nchi huru

Maelfu ya wananchi wa Sudan Kusini wamekusanyika kushuhudia kupandishwa kwa bendera mpya ya nchi hiyo kuashiria kupata uhuru wake, katika mji mkuu Juba.
Rais wa Sudan Omar al-Bashir na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ban Ki-moon ni miongoni mwa wageni waliohudhuria shughuli hiyo.
Sudan Kusini limekuwa taifa jipya duniani usiku wa kuamkia Jumamosi, lengo ambalo limefikiwa kufuatia mkataba wa amani wa mwaka 2005 uliomaliza mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yaliyodumu kwa miaka mingi.
Sudan lilikuwa taifa la kwanza kuitambua Rasmi Sudan Kusini.
Uhuru wa Sudan Kusini unafuatia mzozo kati ya Kusini na Kaskazini uliosababisha vifo vya watu milioni 1.5.
Sherehe za uhuru zilianza saa sita kamili saa za Sudan Kusini mjini Juba. Saa iliyowekwa katikati ya jiji ilipotimu saa sita kamili, wimbo mpya wa taifa ulipigwa kupitia televisheni ya taifa hilo.
Sudan Kusini inakuwa taifa la 193, na kutambuliwa na Umoja wa Mataifa, na pia kuwa taifa la 54 barani Afrika.